Swahili New Testament Bible

Luke 13

Luke

Return to Index

Chapter 14

1

Siku moja ya Sabato, Yesu alikwenda kula chakula nyumbani kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo; watu waliokuwapo hapo wakawa wanamchunguza.

2

Mbele yake Yesu palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa na ugonjwa wa kuvimba mwili.

3

Yesu akawauliza walimu wa Sheria na Mafarisayo, "Je, ni halali au la kumponya mtu siku ya sabato?"

4

Lakini wao wakakaa kimya. Yesu akamshika huyo mgonjwa, akamponya, akamwacha aende zake.

5

Halafu akawaambia, "Ni nani kati yenu ambaye mtoto wake au ng`ombe wake akitumbukia shimoni, hangemtoa hata kama ni siku ya Sabato?"

6

Nao hawakuweza kumjibu swali hilo.

7

Yesu aliona jinsi wale walioalikwa walivyokuwa wanajichagulia nafasi za heshima, akawaambia mfano:

8

"Kama mtu akikualika arusini, usiketi mahali pa heshima isije ikawa amealikwa mwingine mheshimiwa kuliko wewe;

9

na mwenyeji wenu ninyi wawili atakuja na kukwambia: `Mwachie huyu nafasi.` Hapo utaaibika mbele ya wote na kulazimika kwenda kuchukua nafasi ya mwisho.

10

Bali ukialikwa kwenye karamu, keti mahali pa mwisho, ili mwenyeji wako atakapokuja akwambie: `Rafiki, njoo hapa mbele, mahali pazuri zaidi.` Hapo utakuwa umeheshimika mbele ya wote wanaoketi pamoja nawe.

11

Kwa maana yeyote anayejikweza atashushwa, na anayejishusha, atakwezwa."

12

Halafu akamwambia na yule aliyemwalika, "Kama ukiwaandalia watu karamu mchana au jioni, usiwaalike rafiki zako au jamaa zako au jirani zako walio matajiri, wasije nao wakakualika nawe ukawa umelipwa kile ulichowatendea.

13

Badala yake, unapofanya karamu, waalike maskini, vilema viwete na vipofu,

14

nawe utakuwa umepata baraka, kwa kuwa hao hawana cha kukulipa. Maana Mungu atakupa tuzo lako wakati watu wema watakapofufuka."

15

Mmoja wa wale waliokuwa wameketi pamoja na Yesu akasema, "Ana heri mtu yule atakayekula chakula katika Ufalme wa Mungu."

16

Yesu akamjibu, "Mtu mmoja alifanya karamu kubwa, akaalika watu wengi.

17

Wakati wa karamu ulipofika alimtuma mtumishi wake awaambie walioalikwa, `Njoni, kila kitu ni tayari.`

18

Lakini wote, kwa namna moja, wakaanza kuomba radhi. Wa kwanza akamwambia mtumishi: `Nimenunua shamba, kwa hiyo sina budi kwenda kuliangalia; nakuomba uniwie radhi.`

19

Mwingine akasema: `Nimenunua ng`ombe jozi tano wa kulima; sasa nimo njiani kwenda kuwajaribu; nakuomba uniwie radhi.`

20

Na mwingine akasema: `Nimeoa mke, kwa hiyo siwezi kuja.`

21

Mtumishi huyo akarudi na kumwarifu bwana wake jambo hilo. Yule mwenye nyumba alikasirika, akamwambia mtumishi wake: `Nenda upesi kwenye barabara na vichochoro vya mji, uwalete hapa ndani maskini, viwete, vipofu na waliolemaa.`

22

Baadaye, mtumishi huyo akasema: `Bwana mambo yamefanyika kama ulivyoamuru, lakini bado iko nafasi.`

23

Yule bwana akamwambia mtumishi: `Nenda katika barabara na vichochoro vya mji uwashurutishe watu kuingia ili nyumba yangu ijae.

24

Kwa maana, nawaambieni, hakuna hata mmoja wa wale walioalikwa atakayeonja karamu yangu."`

25

Hapo, makundi mengi yakawa yanaandamana pamoja na Yesu. Basi, akawageukia akawaambia,

26

"Mtu yeyote akija kwangu, asipowachukia baba na mama yake, mke wake, watoto, ndugu na dada zake, naam, hata na nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

27

Mtu asipochukua msalaba wake na kunifuata hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

28

Kwa maana, ni nani miongoni mwenu ambaye akitaka kujenga mnara hataketi kwanza akadirie gharama zake ili ajue kama ana kiasi cha kutosha cha kumalizia?

29

La sivyo, baada ya kuweka msingi na kushindwa kumaliza, watu watamcheka

30

wakisema: `Mtu huyu alianza kujenga, lakini hakumalizia.`

31

"Au, ni mfalme gani ambaye, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, hataketi kwanza chini na kufikiri kama ataweza, kwa askari wake elfu ishirini?

32

Kama anaona hataweza, atawatuma wajumbe kutaka masharti ya amani wakati mfalme huyo mwingine angali mbali.

33

Vivyo hivyo, basi, hakuna hata mmoja wenu atakayekuwa mwanafunzi wangu kama asipoachilia kila kitu alicho nacho.

34

"Chumvi ni nzuri; lakini ikipoteza ladha yake, itakolezwa na nini?

35

Haifai kitu wala kwa udongo wala kwa mbolea. Watu huitupilia mbali. Sikieni basi, kama mna masikio!"

Luke 15

 

 

 

Please Click the Ads.

Clicking the Ads helps us to keep this free Bible website open for everyone.

Thanks!

 

 

 

HTMLBible Software - Public Domain Software by johnhurt.com

 


Other Items are Available At These Sites: